MATHAYO 5 : 14 -16
Jukumu ninajitwika, kushukuru wetu mu’mba,
Kutuwezesha kufika, kwenye takatifu jumba,
Nadhani ninasikika, nanyi nyote kwenye jumba,
Mimi hapa nimefika, maadili kuyalumba
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,
Katika mathayo tano, anza arobatashara,
Pitia kumi na tano, fikia sitatashara,
Yatoa mwema mfano, wakutuweka imara,
Naomba tuwe mifano,
tuyaache masihara,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,
Twafananishwa na mji, ul’ojengwa mlimani,
Ni wengi watazamaji, huuona duniani,
Jalali hutuhitaji, tuwe mwanga maishani,
Aidha hutuhitaji, tumulike hadharani,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,
Ikiwa tumeokoka, twonyeshe wokovu wetu,
Tuweze kuheshimika, katika maisha yetu,
Na tuwe wa kuigika, katika matendo yetu,
Tuwe wa kutajika, kwa wema ulonyumetu,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,
Tusiwe watu wa chuki, tusije dharauliwa,
Tufaane kwenye dhiki, mola ataabudiwa,
Tuombeane riziki, na tena kubarikiwa,
Tusiunge ufasiki, kwani tumeteuliwa,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,
La Mola husema buku, tusiwe wa kugawanya,
Tusiwe wenye udaku, na wenzetu kuwasinya,
Tusiwe watu wa chuku, midomo ya kusengenya,
Tuzipige marufuku, akili za kudanganya,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,
Naomba mnipe mwanya, niende nyumbani kwangu,
N’ambie babu na nyanya, na hata wazazi wangu,
Liwapasao kufanya, ili waitwe wa Mungu,
Machache nimewakanya, tii ushauri wangu,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie.
SHUKURANI
Malenga Marc Karash