MPENZI WANGU
Tangu nilipokuona, ninahisi nina deni,
Kuna jambo sijanena, laninyima burudani,
Najaribu kulinena, sasa mara elfeni,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,
Nimeona wasichana, wengi toka utotoni,
Kama wewe sijaona, kipenzi hurulaini,
Picha yako naiona, usiku usingizini,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,
Umbo limebabatana, hasa pale kifuani,
Nitaishi kulighana, siku zangu maishani,
Na sura yaambatana, na rangi kote mwilini,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,
Nywele zako umechana, zinafika mabegani,
Usemi wako mwanana, na tabasamu usoni,
Utulivu wa kinena, yote hayo buruhani,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,
Mikono yako kimwana, misafi tena laini,
Nyuma wapendeza sana, watia fisi mbioni,
Na macho ya kiborana, yang’aa bila miwani
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,
Muda wangu wa kunena, umefika ukingoni,
Ni mengi sijayanena, kutoa
yalo moyoni,
Sababu wewe kimwana, penzi lako li moyoni,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,
SHUKURANI
Malenga Marc Karash
No comments:
Post a Comment