Thursday, 1 March 2018

SHAIRI KWA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA.



KURUNZI BORA

Hamjambo wanafunzi, karibu hapa shuleni,
Hivi leo kiburunzi, siku yenu ugenini,
Nimekataa kihunzi, nawa’mbia hadharani,
Iliyo bora kurunzi, ni kusoma upilini,

Mmeviruka viunzi, tangu pale msingini,
Mtawawahi wapenzi, mkiwa hapa shuleni,
Mtasimulia tenzi, lakini mkumbukeni,
Iliyo bora kurunzi, ni kusoma upilini,

Myakumbuke majonzi, ya wazazi viamboni,
Wengine wakurugenzi, wengine wa mashambani,
Lakini wanayaenzi, masomo ya upilini,
Iliyo bora kurunzi, ni kusoma upilini,

Hapa tuna wakufunzi, walimu ‘toka vyuoni,
Aidha tuna walinzi, mliopata langoni,
Pia tuna wanafunzi, watakao wa’mbieni,
Iliyo bora kurunzi, ni kusoma upilini,

Nidhamu na muienzi, musiruke adhabuni,
Sikio lisife ganzi, ushauri sikizeni,
Leo tuanze utenzi, wa kufaidi mwishoni,
Iliyo bora kurunzi, ni kusoma upilini,

Kalamu yapiga kwenzi, nakudai niacheni,
Sikuifunga tanzi, itabidi nikomeni,
Isije leta kitanzi, nikidhani ni utani,
Iliyo bora kurunzi, ni kusoma upilini,

SHUKURANI
Malenga Marc Karash

No comments:

Post a Comment

HADITHI YA KUSISIMUA

ANN NA MUTUVIE Jina lake ni Ann. Sura anayo ndio, umbo analo ndio pia tabasamu lake lingemvutia kila mtu kwenye gari waliyoisafiri. M...