Thursday, 1 March 2018

UMOJA
`Ushauri nilisaka, na jalali nikamwomba,
Anijalie fanaka, walau neze kulumba,
Nashukuru mmefika, tulia niwape dumba,
Nadhani ninasikika, nanyi nyote kwenye chumba,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

Boma lenye utengano, huishi kufitiniwa,
Nchi yenye utengano, itaishi kudhuriwa,
Tuki’ga utangamano, nchi itaheshimiwa,
Lakini kwa makinzano, nchi itakashifiwa,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

Ugaidi kila kona, milipuko ya kutisha,
Tusipo sisi ungana, magaidi watatisha,
Lakini tukiungana, ugaidi ‘takomesha,
Panapo wal’oungana, huwa ni bora maisha,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

Wanasiasa tu’ngane, halafa na serikali,
Uchanya tuambiane, na ukweli tujadili,
Uhasi tuambiane, kwa njia ilo halali,
Wenzetu tusiwakane, wakikumbwa na ajali,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

Tuungane wanadini, isilamu kirisito,
Kazikazi na kusini, tu’ngane tuzime moto,
Mikakati ya wahuni, tuizime iwe ndoto,
Tutangamane halani, wazazi pia watoto,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

Umoja ni ushujaa, wakenya nawambieni,
Nchi yetu imejaa, mikasa aidha zani,
Kuna majanga ya njaa, mioto pia uhuni,
Ili sisi kujifaa, tuungane hadharani,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

Ukurasa memaliza, memaliza ku’nganisha,
Naona ikija giza, nuru inadidimisha,
Kesho nawahimiza, muweze kunikumbusha,
Nipate kuumaliza, mswada wa ku’nganisha,
Umoja ni cheti bora, cha kupata mambo yote.

SHUKURANI
Malenga: Marc-Karash
0707090505

No comments:

Post a Comment

HADITHI YA KUSISIMUA

ANN NA MUTUVIE Jina lake ni Ann. Sura anayo ndio, umbo analo ndio pia tabasamu lake lingemvutia kila mtu kwenye gari waliyoisafiri. M...