ANN NA MUTUVIE
Jina lake ni
Ann. Sura anayo ndio, umbo analo ndio pia tabasamu lake lingemvutia kila mtu
kwenye gari waliyoisafiri. Mutuvie alikaa kimya na kujifanya hayaoni hayo. Ann
alishangaa Mutuvie ni mvulana aina gani, imani yake ni gani na wapi akaazima
hisi zake za kiume. Itakuwaje wamesafiri
takribani kilomita tatu sasa bila ya kusemezana chochote. Alitamani gari hili
lingekuwa na kiti cha ziada angehamia pale amwache mvulana wetu. Alifungua begi
yake ya mkononi iliyokuwa juu ya mapaja
yake huku ameikumbatia tumboni pake. Alitoa wanja na kioo cha kiduara chenye
ngozi ya rangi ya kijani. Alipangusa pangusa mboni zake huku akijitazama kwenye
kioo na baadaye kurudisha bidhaa zake. Hakutumia wanja. Alitazama juu kidogo
kama anayewaza jambo Fulani. Alijivuta nyuma kitini na kuvuta sketi yake fupi
kujaribu kuficha mapaja yake yaliyoachwa wazi. Alikuwa amevalia mini sketi ya
rangi ya samawati na shati nyeupe iliyoshindwa kuficha rangi nyekundu ya
kanchiri. Kichwani alisongwa mtindo wa sokota.
Kwa upande
mwingine, Mutuvie alijifanya ametulia ila alikuwa na mshangao na wasiwasi
mwingi. “panya anafanya nini ndani ya begi langu? Alipitia wapi kuingia humo? Nimesafiri
naye kwa muda gani?” Hayo ni baadhi ya maswali aliyokuwa anajiuliza kijana
Mutuvie. Kusema ukweli, Mutuvie alivutiwa na urembo wa Ann. Alichukua karibu
dakika ishirini tangu gari ling’oe nanga akifikiria ataanza vipi kumsemeza Ann.
Alikuwa kwenye kipindi cha kuuguza majeraha aliyopata baada ya kupewa talaka na
mpenzi wake wa muda mrefu baada ya muhula wa mwisho chuoni. Fursa hii, aliiona
mwafaka kutibu majeraha yake ya kimapenzi. Baada ya dakika hizo ishirini,
alipata wazo. Aliamua kuchukua rununu yake, aandike ujumbe kuhusu hisia zake
kwa Ann kisha amwache Ann asome kwenye kiwaa cha simu hiyo. Alistaajabu ya Musa
alipofungua begi lake la begani lenye rangi ya udongo. Hakustaajabishwa na
usafi wa suruali lake jeusi la kiofisi
wala usafi wa shati lake jeupe la kiofisi bali alistaajabishwa na panya mkubwa
kimo cha paka aliyekuwa anatawala ndani ya begi lake. Aliharrakisha kufunga
begi hilo. Hakutaka Yule panya atoke kwanza ili asijiaibishe kwa Ann na pili
asiwashtue abiria wengine. Alifunga begi
lake na kukaa kimya hata hayaoni haya yote Ann anayoyafanya.
Mutuvie
anakumbuka tu akimwambia Ann “safari salama.” Njiani alipanda na kushuka,
kuelekea nyumbani kwao. Alikuwa na majukumu mawili mbele yake. Kwanza, ingebidi
aeleze wazazi wake kumhusu panya aliye ndani ya begi lake. Angetaka yeye na wazazi wake wasaidiane kufikiri sababu
ya panya kuingia begini mle. Pili, angeeleza wazazi wake na mwingine yeyote
kuhusu kufuzu kwake katika mitihani yote pale chuoni. Alikuwa katika orodha ya
waliotarajiwa kuhitimu katika shahada ya kwanza wiki iliyofuata. Huo ndio
ujumbe uliomfanya kuelekea nyumbani.
Mutuvie alipofika
kwenye lango la boma yao, mambo yalibadilika. Ingawaje yeye sio mgeni, mbwa wao
hubweka dhidi ya mtu yeyote apitiaye lango la boma hiyo. Siku hiyo hakubweka
wala hakuonekana. Jambo hili lilimtia Mutuvie wasiwasi. Alipiga hodi
asikaribishwe na yeyote. Wingu la woga lilitanda manthari ya pale. Ndege na
wadudu walitimya ndimi zao kusubiri kitakacho jitokeza. Chumba cha wazazi wa
Mutuvie, chumba cha kupikia na kile chake vyote vilikuwa milango wazi.
Alitarajia watu wawili pale nyumbani, baba na mama tu. Alishangaa ni nani
mwingine anamiliki ufunguo wa chumba chake isipokuwa yeye pekee. Aliamua
kuitana ili kuondoa utata uliomkumba. Sauti yake haikujibiwa na mtu wala
mwangwi. Panya aliyekuwa begini mwake alitikisatikisa begi kana kwamba anaomba
uhuru wa kutorokea yaliyo mbele ya kijana wetu. Mwili wa Mutuvie uliganda kwa
woga. Kama mwanamume, Mutuvie alijijasirisha kufululiza hadi kwa chumba chake.
Maskini kijana wetu hata kabla kuingia ndani, alipatana na damu nyingi iliyotapakaa
karibu na mlango wa nyumba. Alipigwa na butwaa na kuangusha begi chini kisha
akafutuka kuelekea chumba cha kupikia huku akiitana mama, mama. Karibu na
mlango wa chumba cha kupikia aidha alipata damu matapishi yametapakaa pale.
Ardhini palikuwa na mikwaruzo ishara kwamba palikuwa na mng’ang’ano dhidi ya
viumbe wawili. Alichungulia ndani huku akiita
mama. Upande wa ndani vyombo kadhaa vilikuwa vimeanguka ovyo ovyo na
maji kutapakaa kila mahali. Alikimbilia chumba cha wazazi huku machozi
yanamtiririka. Kukaribia mlango wa kile chumba, mlango ulijifunga kwa kishindo.
Alijaribu kuufungua huku hakiita baba na mama. Aliusukuma kwa kutumia bega lake
na goti la mguu wake wa kulia lakini komeo ilikuwa ishawekwa kutoka ndani.
Aliugonga gonga kwa vishindo huku
akiendelea kuita lakini hakupata jibu. Alipoangaza macho kusaka silaha ya
kuvunja mlango, aliona karatasi ilioandikwa PIPA LA TAKATAKA. Fahamu zilikuwa
zimemtoka lakini alijipata karibu na pipa la taka taka.Ndani ya pipa hilo
hakukuwa na chochote ila jeneza lililobeba kiunzi cha mifupa ( skeleton). Kabla
hajafanya lolote, kile kiunzi kilipasa sauti. “Mwanangu, mimi ni baba yako na
usinikaribie…..,” “baaaa… “ ‘ usiniite!’ sauti ilikatiza kijana wetu. “ Niko
tayari kukutoa kafara lakini kwanza enda zizini umsalimie mama yako. Harrakisha!
Sauti iliendelea. Mutuvie alijihisi ahera. Ile sauti ilimtia gia ya hadi
zizini. Zizini alipata kiunzi kingine cha mifupa. Alianza kwenda kisengesenge
lakini sauti ilimwita. “Mutuvie mwanangu mbona waniondokea? Mimi ni mama yako
usiogope.” Miguu ya Mutuvie ilikufa ganzi na akazirai. Akiwa pale chini kile
kiunzi kilinyosha mkono juu yake na kusema.”LALA SALAMA.”
Mutuvie aligutushwa
na mlio wakitanda. Alijipata amelala mvunguni mwa kitanda na juu yake gondoro
limeandikwa LALA SALAMA. Juu ya kitanda ni mgeni wake Winnie aliyekuwa amemtembelea
usiku wa kuamkia siku hiyo. Alipotazama
akrabu ya saa ukutani,ilikuwa saa moja na dakika ishirini asubuhi. Alikuwa amechelewa
kunywa dawa ya asubuhi kwa dakika ishirini. Alikimbilia begi lake la rangi ya
udongo liliyokuwa kochini na kulifungua kwa makini. Alitoa kidonge cha dawa na
kukibwagia kinywani. Alikimeza bila ya maji na kuangaza macho yake
kitandani.Mgeni wake alikuwa angali
amelala fofofo. Ametia mguu wake mmoja kwenye mini sketi yake ya samawati.
Kanchiri nyekundu ilikuwa chini karibu na kochi nayo blausi yake nyeupe iko juu
ya kochi.” Kitandani nilitoka lini? Labda mototo wa wenyewe aliniskia niking’ang’ana
na ndoto zangu mle mvunguni? Kweli nilitoa usaidizi alioutaka mgeni wangu
Winnie?” Mutuvie alianza maswali.