CHANGAMOTO ZA MAISHA
Safari nimeshafunga, katika maisha yangu,
Mbele mbele ninasonga, nifikie ndoto zangu,
Hasimu wakinitenga, natuliza moyo wangu,
Changamoto za maisha,
haziui ndoto zangu,
Tangu nikiwa mchanga, maisha ni dungudungu,
Riziki ninaidanga, huku nikiomba Mungu,
Wale wananisimanga, wasiue ari yangu,
Changamoto za maisha,
haziui ndoto zangu,
Ukata umebiringa, wengi wa umri wangu,
Ndoto zao kabananga, wakabaki na uchungu,
Lakini nauchabanga, hautanifunga pingu,
Changamoto za maisha,
haziui ndoto zangu,
Matatizo yamenisonga, katika maisha yangu,
Rafiki wananibonga, watangaza siri zangu,
Wengine wananikenga, wachanganye bongo zangu,
Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu,
Hela zanipiga chenga, sijalipa karo yangu,
Mwenye nyumba ‘meifunga, na kupa wake ufungu,
Leo nakoma kupanga, nisake nyumbani kwangu,
Changamoto za maisha,
haziui ndoto zangu,
Beti zangu nimefunga, niende nyumbani kwangu,
Ndugu nimeshawagunga, katika hayo mafungu,
Nangoja mvue kanga, muige msemo wangu,
Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu.
SHUKURANI
Malenga Marc Karash.
No comments:
Post a Comment