Sunday, 3 November 2019

HADITHI YA KUSISIMUA


ANN NA MUTUVIE
Jina lake ni Ann. Sura anayo ndio, umbo analo ndio pia tabasamu lake lingemvutia kila mtu kwenye gari waliyoisafiri. Mutuvie alikaa kimya na kujifanya hayaoni hayo. Ann alishangaa Mutuvie ni mvulana aina gani, imani yake ni gani na wapi akaazima hisi zake za kiume.  Itakuwaje wamesafiri takribani kilomita tatu sasa bila ya kusemezana chochote. Alitamani gari hili lingekuwa na kiti cha ziada angehamia pale amwache mvulana wetu. Alifungua begi yake ya mkononi  iliyokuwa juu ya mapaja yake huku ameikumbatia tumboni pake. Alitoa wanja na kioo cha kiduara chenye ngozi ya rangi ya kijani. Alipangusa pangusa mboni zake huku akijitazama kwenye kioo na baadaye kurudisha bidhaa zake. Hakutumia wanja. Alitazama juu kidogo kama anayewaza jambo Fulani. Alijivuta nyuma kitini na kuvuta sketi yake fupi kujaribu kuficha mapaja yake yaliyoachwa wazi. Alikuwa amevalia mini sketi ya rangi ya samawati na shati nyeupe iliyoshindwa kuficha rangi nyekundu ya kanchiri. Kichwani alisongwa mtindo wa sokota.

Kwa upande mwingine, Mutuvie alijifanya ametulia ila alikuwa na mshangao na wasiwasi mwingi. “panya anafanya nini ndani ya begi langu? Alipitia wapi kuingia humo? Nimesafiri naye kwa muda gani?” Hayo ni baadhi ya maswali aliyokuwa anajiuliza kijana Mutuvie. Kusema ukweli, Mutuvie alivutiwa na urembo wa Ann. Alichukua karibu dakika ishirini tangu gari ling’oe nanga akifikiria ataanza vipi kumsemeza Ann. Alikuwa kwenye kipindi cha kuuguza majeraha aliyopata baada ya kupewa talaka na mpenzi wake wa muda mrefu baada ya muhula wa mwisho chuoni. Fursa hii, aliiona mwafaka kutibu majeraha yake ya kimapenzi. Baada ya dakika hizo ishirini, alipata wazo. Aliamua kuchukua rununu yake, aandike ujumbe kuhusu hisia zake kwa Ann kisha amwache Ann asome kwenye kiwaa cha simu hiyo. Alistaajabu ya Musa alipofungua begi lake la begani lenye rangi ya udongo. Hakustaajabishwa na usafi wa suruali lake jeusi  la kiofisi wala usafi wa shati lake jeupe la kiofisi bali alistaajabishwa na panya mkubwa kimo cha paka aliyekuwa anatawala ndani ya begi lake. Aliharrakisha kufunga begi hilo. Hakutaka Yule panya atoke kwanza ili asijiaibishe kwa Ann na pili asiwashtue abiria wengine.  Alifunga begi lake na kukaa kimya hata hayaoni haya yote Ann anayoyafanya.

Mutuvie anakumbuka tu akimwambia Ann “safari salama.” Njiani alipanda na kushuka, kuelekea nyumbani kwao. Alikuwa na majukumu mawili mbele yake. Kwanza, ingebidi aeleze wazazi wake kumhusu panya aliye ndani ya begi lake. Angetaka  yeye na wazazi wake wasaidiane kufikiri sababu ya panya kuingia begini mle. Pili, angeeleza wazazi wake na mwingine yeyote kuhusu kufuzu kwake katika mitihani yote pale chuoni. Alikuwa katika orodha ya waliotarajiwa kuhitimu katika shahada ya kwanza wiki iliyofuata. Huo ndio ujumbe uliomfanya kuelekea nyumbani.

Mutuvie alipofika kwenye lango la boma yao, mambo yalibadilika. Ingawaje yeye sio mgeni, mbwa wao hubweka dhidi ya mtu yeyote apitiaye lango la boma hiyo. Siku hiyo hakubweka wala hakuonekana. Jambo hili lilimtia Mutuvie wasiwasi. Alipiga hodi asikaribishwe na yeyote. Wingu la woga lilitanda manthari ya pale. Ndege na wadudu walitimya ndimi zao kusubiri kitakacho jitokeza. Chumba cha wazazi wa Mutuvie, chumba cha kupikia na kile chake vyote vilikuwa milango wazi. Alitarajia watu wawili pale nyumbani, baba na mama tu. Alishangaa ni nani mwingine anamiliki ufunguo wa chumba chake isipokuwa yeye pekee. Aliamua kuitana ili kuondoa utata uliomkumba. Sauti yake haikujibiwa na mtu wala mwangwi. Panya aliyekuwa begini mwake alitikisatikisa begi kana kwamba anaomba uhuru wa kutorokea yaliyo mbele ya kijana wetu. Mwili wa Mutuvie uliganda kwa woga. Kama mwanamume, Mutuvie alijijasirisha kufululiza hadi kwa chumba chake. Maskini kijana wetu hata kabla kuingia ndani, alipatana na damu nyingi iliyotapakaa karibu na mlango wa nyumba. Alipigwa na butwaa na kuangusha begi chini kisha akafutuka kuelekea chumba cha kupikia huku akiitana mama, mama. Karibu na mlango wa chumba cha kupikia aidha alipata damu matapishi yametapakaa pale. Ardhini palikuwa na mikwaruzo ishara kwamba palikuwa na mng’ang’ano dhidi ya viumbe wawili. Alichungulia ndani huku akiita  mama. Upande wa ndani vyombo kadhaa vilikuwa vimeanguka ovyo ovyo na maji kutapakaa kila mahali. Alikimbilia chumba cha wazazi huku machozi yanamtiririka. Kukaribia mlango wa kile chumba, mlango ulijifunga kwa kishindo. Alijaribu kuufungua huku hakiita baba na mama. Aliusukuma kwa kutumia bega lake na goti la mguu wake wa kulia lakini komeo ilikuwa ishawekwa kutoka ndani. Aliugonga  gonga kwa vishindo huku akiendelea kuita lakini hakupata jibu. Alipoangaza macho kusaka silaha ya kuvunja mlango, aliona karatasi ilioandikwa PIPA LA TAKATAKA. Fahamu zilikuwa zimemtoka lakini alijipata karibu na pipa la taka taka.Ndani ya pipa hilo hakukuwa na chochote ila jeneza lililobeba kiunzi cha mifupa ( skeleton). Kabla hajafanya lolote, kile kiunzi kilipasa sauti. “Mwanangu, mimi ni baba yako na usinikaribie…..,” “baaaa… “ ‘ usiniite!’ sauti ilikatiza kijana wetu. “ Niko tayari kukutoa kafara lakini kwanza enda zizini umsalimie mama yako. Harrakisha! Sauti iliendelea. Mutuvie alijihisi ahera. Ile sauti ilimtia gia ya hadi zizini. Zizini alipata kiunzi kingine cha mifupa. Alianza kwenda kisengesenge lakini sauti ilimwita. “Mutuvie mwanangu mbona waniondokea? Mimi ni mama yako usiogope.” Miguu ya Mutuvie ilikufa ganzi na akazirai. Akiwa pale chini kile kiunzi kilinyosha mkono juu yake na kusema.”LALA SALAMA.”

Mutuvie aligutushwa na mlio wakitanda. Alijipata amelala mvunguni mwa kitanda na juu yake gondoro limeandikwa LALA SALAMA. Juu ya kitanda ni mgeni wake Winnie aliyekuwa amemtembelea  usiku wa kuamkia siku hiyo. Alipotazama akrabu ya saa ukutani,ilikuwa saa moja na dakika ishirini asubuhi. Alikuwa amechelewa kunywa dawa ya asubuhi kwa dakika ishirini. Alikimbilia begi lake la rangi ya udongo liliyokuwa kochini na kulifungua kwa makini. Alitoa kidonge cha dawa na kukibwagia kinywani. Alikimeza bila ya maji na kuangaza macho yake kitandani.Mgeni wake alikuwa  angali amelala fofofo. Ametia mguu wake mmoja kwenye mini sketi yake ya samawati. Kanchiri nyekundu ilikuwa chini karibu na kochi nayo blausi yake nyeupe iko juu ya kochi.” Kitandani nilitoka lini? Labda mototo wa wenyewe aliniskia niking’ang’ana na ndoto zangu mle mvunguni? Kweli nilitoa usaidizi alioutaka mgeni wangu Winnie?” Mutuvie alianza maswali.

Wednesday, 30 October 2019

SHAIRI KUHUSU MGOMO

                                      SHULE YA KINYAA
uongozi wenye haki, nimeishi kutamani,
lakini hausikiki, hata nikiwa makini,
ndo mana mi ni shabiki, wa waendao nyumbani,
shule yetu ya kinyaa, taa leo kawa moto,

unapowatamalaki, tajiri na maskini,
usiwaulize laki, walipe pasi na deni,
unawapa nne wiki, kuwatoa darasani,
shule yetu ya kinyaa, taa leo kawa moto,

hili haliaminiki, kutimu sasa faini,
ambayo hailipiki, kaongeza Firauni,
inafaa mshaliki, ndo turudi darasani,
shule yetu ya kinyaa, taa leo kawa moto,

usifosi halaiki, wapite njia fulani,
nafikiri wana haki, kupita barabarani,
usiwatie hamaki, kuwafosi jukwaani
shule yetu ya kinyaa, taa leo kawa moto,

huku kumejaa taki, takataka na sabuni,
eti mliwataliki, wafanyakazi kwa nini,
sasa tumesadiki, sisi hamtujalini,
shule yetu ya kinyaa, taa leo kawa moto,

kweli haiaminiki, ukuta wa nyayo chini,
karao wawe lukuki, sisi tuko milioni,
wakitumia bunduki, sisi mawe mikononi,
shule yetu ya kinyaa, taa leo kawa moto.

SHUKURANI
Mtunzi - Marc - Karash
0795936959SHAIRI KUHUSU MUGOMO


Wednesday, 14 November 2018

HASIDI
Nasoma ushairini, Wa malenga Ben Njoka,
Kuhusu mtu fulani, hasidi atambulika,
Sifa yake ndiyo gani, tazama naimulika,
Wakati uko tabani, anakucheka moyoni,
Anakucheka moyoni, tatizo likikufika,
Huzuni anaubuni, pole akizitamka,
Na Kumbe ndani moyoni, hawezi koma kucheka,
Husuda humfitini, akikuona kileleni,
Akikuona kileleni, kwa wema ukisifika,
Atakesha msituni, waganga akiwasaka,
Wakuroge kwa makini, hadi upate kushuka,
Akiulizwa kwa nini, yeye kesi atabuni,
Yeye kesi atabuni, toto lake umebaka,
Akimbilie kotini, kufungua mashtaka,
Na ukishinda kesini, aseme ushikwe haka,
Anataka uwe duni, asikwone na fulani,
Asikwone na fulani, mkila ama kucheka,
Atamwendea jioni, rongo zake kuropoka,
Amsemee jamani, akili zimekuruka,
Usimpende fulani, atakurushia jini,
Atakurushia jini, akili itakuruka,
Akuseme kijijini, kono lako karefuka,
Pembe zote duniani, matope atakupaka,
Ben Njoka asemeni, hasidi sio shetani,
Hasidi sio shetani, nadhani yaeleweka,
Aweza kuwa jirani, ushindwe kumuepuka,
Una hasidi uani, wewe ishi kukumbuka,
Nasoma ushairini, wa malenga Ben Njoka,
Mtunzi -Marc karash
Kutoka-Embu
Kijiji -Kwandu -ambai
Simu. -0707090505/0795936965

Thursday, 1 March 2018

SHAIRI KWA WAKRISTO



MATHAYO 5 : 14 -16
Jukumu ninajitwika, kushukuru wetu mu’mba,
Kutuwezesha kufika, kwenye takatifu jumba,
Nadhani ninasikika, nanyi nyote kwenye jumba,
Mimi hapa nimefika, maadili kuyalumba
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,

Katika mathayo tano, anza arobatashara,
Pitia kumi na tano, fikia sitatashara,
Yatoa mwema mfano, wakutuweka imara,
Naomba tuwe  mifano, tuyaache masihara,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,

Twafananishwa na mji, ul’ojengwa mlimani,
Ni wengi watazamaji, huuona duniani,
Jalali hutuhitaji, tuwe mwanga maishani,
Aidha hutuhitaji, tumulike hadharani,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,

Ikiwa tumeokoka, twonyeshe wokovu wetu,
Tuweze kuheshimika, katika maisha yetu,
Na tuwe wa kuigika, katika matendo yetu,
Tuwe wa kutajika, kwa wema ulonyumetu,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,

Tusiwe watu wa chuki, tusije dharauliwa,
Tufaane kwenye dhiki, mola ataabudiwa,
Tuombeane riziki, na tena kubarikiwa,
Tusiunge ufasiki, kwani tumeteuliwa,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,

La Mola husema buku, tusiwe wa kugawanya,
Tusiwe wenye udaku, na wenzetu kuwasinya,
Tusiwe watu wa chuku, midomo ya kusengenya,
Tuzipige marufuku, akili za kudanganya,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie,

Naomba mnipe mwanya, niende nyumbani kwangu,
N’ambie babu na nyanya, na hata wazazi wangu,
Liwapasao kufanya, ili waitwe wa Mungu,
Machache nimewakanya, tii ushauri wangu,
Tusiwashe zetu taa, halafu tufunikie.

SHUKURANI
Malenga Marc Karash

SHAIRI KUHUSU VIPAJI



KIPAJI NI NGUVU
Kabla jimbi kuwika, nashukuru wetu mu’mba,
Kutuwezesha kufika, kwenye takatifu jumba,
Nadhani ninasikika, nanyi nyote kwenye jumba,
Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani,

Vipaji vipaji kaka, hupeanwa naye mu’mba,
Vipaji vya kutajika, kucheza ama kuimba,
Vingine vya kusifika, kuchora ama kulumba,
 Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani,

Mola ‘liona mwafaka, nisiitwe ombaomba,
Kipaji akanitwika, maishangu kuyapamba,
Mashairi naandika, Januari hadi Disemba,
 Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani,

Shairi nikiandika, linakuwa kama dumba,
Mamia waelimika, nakwacha zao kasumba,
Sasa ni wakuigika, hakika si kujigamba,
Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani,

Nasema leo hakika, kama wajua kuimba,
Uimbe ukisikika, usiimbe kwenye chemba,
Sababu ukisikika, sifa zako zitatamba,
Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani,

Nasema leo hakika, kama wewe ni Lomba,
Ama ulibahatika, na unajua kulumba,
Onekana na sikika, ukilomba ukilumba,
 Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani,

 Kalamu nimeiweka, nakoma usemi wangu,
Sasa imeeleweka, kwenye aridhi na mbingu,
Kila mtu ameshika, kipaji toka kwa Mungu,
Kipaji changu ni nguvu, na kurunzi maishani.

SHUKURANI
 Malenga Marc Karash.

SHAIRI KWA WOTE



CHANGAMOTO ZA MAISHA
Safari nimeshafunga, katika maisha yangu,
Mbele mbele ninasonga, nifikie ndoto zangu,
Hasimu wakinitenga, natuliza moyo wangu,
 Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu,

Tangu nikiwa mchanga, maisha ni dungudungu,
Riziki ninaidanga, huku nikiomba Mungu,
Wale wananisimanga, wasiue ari yangu,
 Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu,

Ukata umebiringa, wengi wa umri wangu,
Ndoto zao kabananga, wakabaki na uchungu,
Lakini nauchabanga, hautanifunga pingu,
 Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu,

Matatizo yamenisonga, katika maisha yangu,
Rafiki wananibonga, watangaza siri zangu,
Wengine wananikenga, wachanganye bongo zangu,
Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu,

 Hela zanipiga chenga, sijalipa karo yangu,
Mwenye nyumba ‘meifunga, na kupa wake ufungu,
Leo nakoma kupanga, nisake nyumbani kwangu,
 Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu,

Beti zangu nimefunga, niende nyumbani kwangu,
Ndugu nimeshawagunga, katika hayo mafungu,
Nangoja mvue kanga, muige msemo wangu,
Changamoto za maisha, haziui ndoto zangu.

SHUKURANI
Malenga Marc Karash.

SHAIRI KWA MPENZI



MPENZI WANGU
Tangu nilipokuona, ninahisi nina deni,
Kuna jambo sijanena, laninyima burudani,
Najaribu kulinena, sasa mara elfeni,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,

Nimeona wasichana, wengi toka utotoni,
Kama wewe sijaona, kipenzi hurulaini,
Picha yako naiona, usiku usingizini,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,

Umbo limebabatana, hasa pale kifuani,
Nitaishi kulighana, siku zangu maishani,
Na sura yaambatana, na rangi kote mwilini,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,

Nywele zako umechana, zinafika mabegani,
Usemi wako mwanana, na tabasamu usoni,
Utulivu wa kinena, yote hayo buruhani,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,

Mikono yako kimwana, misafi tena laini,
Nyuma wapendeza sana, watia fisi mbioni,
Na macho ya kiborana, yang’aa bila miwani
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,

Muda wangu wa kunena, umefika ukingoni,
Ni mengi sijayanena, kutoa  yalo moyoni,
Sababu wewe kimwana, penzi lako li moyoni,
Na leo nimekazana, nikwambie hadharani,

SHUKURANI
Malenga Marc Karash

HADITHI YA KUSISIMUA

ANN NA MUTUVIE Jina lake ni Ann. Sura anayo ndio, umbo analo ndio pia tabasamu lake lingemvutia kila mtu kwenye gari waliyoisafiri. M...